WATU WASIOJULIKANA WAVAMIA OFISI ZA WAKILI WA MANJI

Polisi wakiwa eneo la tukio.

Ofisi ya mawakili ya Prime Attorneys imevamiwa usiku wa manane na watu wasiojulikana ambao wameiba kasiki lenye fedha na nyaraka. Mmoja wa mawakili katika ofisi hiyo,  Hudson Ndusyepo amesema ofisi yao imevunjwa na tayari ameenda polisi kutoa taarifa.

Ndusyepo ambaye ni miongoni mwa mawakili wanaomtetea mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji katika kesi ya uhujumu uchumi, amesema kabla ya wizi huo, waliohusika walimfunga mlinzi kwa kamba.

 

Milango ilivyovunjwa.

Kampuni ya Prime Attorneys katika tovuti yake inaeleza ilianzishwa mwaka 2010. Ofisi za kampuni hiyo zipo Jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza, Upanga jijini Dar es Salaam.

Ofisi hizo zipo kwenye jengo la ghorofa tano lililopo jirani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Ilala.

Leo Asubuhi barabara ya kuingia eneo hilo ilifungwa kwa muda na polisi ambao walitumia magari yao kuziba njia na kuweka uzio wa  utepe wa rangi ya njano.

Wakili Hudson Ndusyepo.

Jengo la Prime House lina ofisi za kampuni mbalimbali, zikiwemo za mawakili, duka la dawa na sehemu ya kufanya mazoezi gym.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni amethibitisha tukio hilo akisema limetokea kati ya saa nane na saa tisa usiku wa kuamkia leo Jumanne.

“Kwa sasa siwezi kusema wahalifu hawa walilenga ofisi gani maana zipo nyingi katika jengo lile. Naomba mtupe nafasi tufanye uchunguzi kisha tutawapa taarifa,” amesema Kamanda Hamduni.

Chanzo : Global Publisher

Facebook Comments

You might also like More from author

Leave A Reply

Your email address will not be published.