VIDONDA VYA TUMBO NA MATIBABU YAKE

Ugonjwa wa vidonda vya tumbo ni ugonjwa ambao unatokana na kumomonyoka (erosion) au kutoboka kwa tabaka la juu la utumbo.

Kwa kawaida tabaka la juu la utumbo hulindwa na ukingo maalum (gastric mucosal barrier) kwa kutengeneza ute (mucous) na alkali za madini ya baikaboneti (bicarbonate ions) dhidi ya tindikali na kimeng’enya (enzyme) cha pepsini.

Mgawanyiko na utengenezwaji wa seli mpya za tabaka la juu la utumbo pamoja na uwepo wa damu ya kutosha ni baadhi ya vigezo vingine vinavyosaidia kulinda tabaka hili na utumbo dhidi ya kumomonyoka au kutoboka.

Kuwepo kwa kigezo chochote kitakachoingiliana na ulinzi dhidi ya tabaka la juu la utumbo hupelekea kumomonyoka kwa tabaka hilo na kusababisha kidonda au vidonda vya tumbo ambavyo huweza kupelekea hata kutoboka kwa utumbo iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Aina za Vidonda vya Tumbo

Kuna aina kuu mbili za vidonda vya tumbo.Aina ya kwanza ni ile inayoathiri tumbo (gastric ulcers) na aina ya pili ni ile inayoathiri utumbo mwembamba wa duodeni (duodenum) ambayo kwa kitaalamu hujulikana kama duodenal ulcers.Aina zote mbili kwa ujumla huitwa peptic ulcers.

Hapo zamani ilikuwepo dhana kwamba msongo wa mawazo (stress) na mlo (diet) husababisha vidonda vya tumbo.Baadaye watafiti wa masuala ya afya ya binadamu waligundua akuwa tindikali izalishwayo tumboni na vimeng’enya vya pepsini vinachangia katika kusababisha vidonda vya tumbo.

Hivi karibuni utafiti umeonyesha kwamba zaidi ya asilimia themanini ya vidonda vya tumbo hutokana na bakteria aitwaye Heliocobacter pylori (H.pylori).Ingawa inasadikika kwamba vigezo vyote hapo juu huchangia kupata vidonda vya tumbo,bakteria H.pylori anasadikiwa kuwa chanzo kikuu katika kusababisha vidonda vya tumbo.

Vidonda vya tumbo (gastric ulcers) na dalili zake

Asilimia kubwa ya waathirika wa aina hii ya vidonda vya tumbo ni watu wenye umri zaidi ya miaka arobaini (40) na wanaume huathirika zaidi kuliko wanawake.Waathirika wa aina hii ya vidonda vya tumbo huwa wembamba kutokana na kutokula wakihofia kupata maumivu pindi walapo chochote.Dalili kubwa ya wagonjwa hawa ni maumivu ya tumbo (chembe).Maumivu yake huwa yenye majira maalum ambapo huanza punde tu mgonjwa alapo chakula na hupungua baada ya chakula kuisha tumboni au kwa kunywa kimiminika chenye alkali.Hamu ya kula huwa nzuri lakini baadhi yao waweza kutapika.Kutapika damu (haematemesis) na kupata choo chenye damu (malaena) huweza kuambatana na aina hii ya vidonda vya tumbo.Uzito wa mwili hupungua kwa kiasi fulani kutokana na kutokula vizuri.Kusambaa kwa maumivu mpaka mgongoni kwaweza kutokea iwapo kidonda kimetoboka na kuhusisha kongosho (pancreas).

Vidonda vya Utumbo mwembamba (duodenal ulcers) na dalili zake

Aina hii ya pili kwa upande mwingine huathiri watu wenye umri chini ya miaka arobaini (40) na kama aina ya kwanza,waathirika wengi ni wanaume.Maumivu, tofauti na aina ya kwanza, hutokea kati ya masaa mawili na nusu hadi manne bada yamlo ambapo chaklula huwa kimeisha tumboni (hunger pains).Maumivu pia hutokea zaidi mapema asubuhi au nyakati za jioni.Nafuu hupatikana kwa kula chakula.

Kutapika hutokea kwa nadra sana kwa wagonjwa wa aina hii.Hata hivyo kutapika damu na kupata choo chenye damu hutokea mara nyingi zaidi kuliko aina ya kwanza.Hamu ya kula kwa wagonjwa wa aina hii huwa nzuri na hupenda kula mara kwa mara hivyo huwa na miili yenye afya nzuri tofauti na wagonjwa wa aina ya kwanza.

Jinsi H.pylori anavyosababisha vidonda vya tumbo
Kuathirika na vimelea vya H.pylori ni kawaida kwa mwanadamu yeyote.Takwimu za Uingereza zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia hamsini ya idadi ya watu wazima wameathirika na bakteria hao.Idadi ni kubwa, zaidi ya asilimia tisini, kwa baadhi ya nchi nyingine.

Hata hivyo ni baadhi tu ya watu kati ya walioathirika na vimelea vya bakteria hawa hupata vidonda vya tumbo.Hakuna sababu za kisayansi zinazoelezea hali hiyo.

Vimelea vya H.pylori huweza kusambaa kupitia chakula na maji.Vimelea vya bakteria hawa pia hupatikana kwenye mate hivyo vyaweza kuambukizwa kupitia kinywa haswa iwapo mtu atabusiana na muathirika wa vimelea hivyo.Watu wengi pia huathirika na vimelea hivi utotoni.

Vimelea vya H.pylori huweza kuishi kwenye ute ulindao tabaka la juu la tumbo na utumbo mpana.Hapo hutengeneza kimeng’enya kiitwacho urease ambacho hupunguza makali ya tindikali izalishwayo na tumbo.Ili kukabiliana na hali hii,tumbo hutengeneza tindikali nyingi zaidi ambayo huathiri tabaka la juu la utumbo.Vimelea hivi pia hudhoofisha ute ulindao tabaka la juu la utmbo hivyo kushindwa kulinda tumbo na utumbo mwembamba sawasawa.

Aidha,vimelea vya H.pylori hujiegesha kwenye seli za tumbo.Hali hii hudhoofisha mfumo wa ulinzi wa tumbo na kusababisha maumivu na hatimaye madhara katika eneo lililoathirika.

Vigezo hatarishi

Vifuatavyo ni vigezo hatarishi ambavyo vyaweza kuongeza uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo.

Madawa ya Kupunguza Maumivu
Dawa hizi ambazo hujulikana pia kama Non Steroidal Anti Inflammatory Drrugs (NSAIDs) hupunguza uwezo wa tumbo kutengeneza ute ulindao utumbo hivyo kuongeza uwezekano wa tabaka la juu la utumbo kumomonyolewa na tindikali.Madawa haya pia yaweza kuathiri upatikanaji wa damu ya kutosha tumboni na uwezo wa mwili haswa utumbo kutengeneza seli mpya.Dawa hizi ambazo hutumika kutibu maumivu ya kichwa na misuli ni Aspirin, Ibuprofen n.k

Sababu za kijenetiki
Historia ya kuwepo kwa kwa vidonda vya tumbo katika ukoo au familia yaweza kuchangia ndugu wa ukoo au familia husika kupata vidonda vya tumbo.Pia, tafiti zimeonyesha uhusiano kati ya watu wenye kundi la damu la O (blood group O) na uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo.

Uvutaji wa sigara
Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuongezeka kwa uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo kutokana na kuvuta sigara.Uvutaji wa sigara huchelewesha kupona kwa kidonda na huchangia kutokea tena kwa kidonda.

Unywaji pombe
Kama ilivyo sigara, pombe huathiri tabaka la utumbo na kupunguza utengenezwaji wa ute ulindao tabaka hilo.

Kafeini (Caffeine)
Kafeini ambayo hupatikana kwenye baadhi ya vinywaji kama soda, kahawa n.k huchangamsha utengenezaji wa tindikali tumboni ambayo hutonesha kidionda kilichopo.
Msongo wa Mawazo
Msongo wa mawazo hausababishi vidonda vya tumbo badala yake huongeza maumivu kwenye kidonda kilichopo.Hufanya hivyo kwa kuongeza zaidi utengenezwaji wa tindikali tumboni.

Uchunguzi na Matibabu
Uchunguzi hujikita zaidi kwenye kuona iwapo utumbo umeathirika na kidonda (vidonda) na pia kwa kuthibitisha uwepo wa vimelea vya bakteria wa H.pylori.
Uchunguzi iwapo utumbo umeathirika na vidonda (endoscopy) hufanywa kwa kutumia tyubu maalum iingizwayo kwenye njia ya chakula hadi kwenye utumbo mwembamba.Kipande cha nyama (biopsy) ya tabaka la juu la utumbo chaweza kuchukuliwa kwa uchunguzi zaidi kwenye hadubini iwapo kuna vimelea vya H.pylori au saratani.
Baadhi ya majaribio maalum kugundua uwepo wa vimelea vya H.pylori ni pamoja na kipiomo cha damu (serology), kipimo cha kupumua urea (urea breath test), kipimo cha kugundua kingamwili kwenye choo (stool antigen test) n.k

Matibabu hujumuisha dozi ya dawa tatu za mseto.Mbili za kiuavijasumu (antibiotic) na moja dhidi ya tindikali (proton pump inhibitor) kwa muda wa juma moja au zaidi.

Ushauri
Ni vyema kumuona daktari ili ufanyiwe uchunguzi na kupatiwa tiba sahihi iwapo una dalili zilizotajwa hapo juu.
Pia ni muhimu kuzingatia dozi kwa kunywa dawa katika muda uliopangwa na kumaliza dozi hata baada ya dalili (maumivu) kupotea.

Ugonjwa wa vidonda vya tumbo tofauti na inavyodhaniwa waweza kupona kabisa kama magonjwa mengine.
Madhara kama kutoboka kwa utumbo,kuvuja damu, kuziba kwa tumbo na saratani ya tumbo yanaweza kutokea iwapo tiba haitatolewa katika muda muafaka

Facebook Comments

You might also like More from author

Leave A Reply

Your email address will not be published.