SIRI ILIYOPO KATIKA KUISHI TABIA YAKO NA FURAHA YAKO

0

Kuonyesha uhalisia wako siyo kosa kwani ipo nguvu ya kipekee katika kuonyesha uhalisia wako. Lakini inakuaje kama dunia inayokuzunguka haiependezwi na hali hiyo?

Kwa mnaojitahidi kuficha tabia zenu za asili ili mradi tu muifurahishe dunia, tafadhali naomba mniruhusu niwapige ngumi za uso.

Ukitaka kuwa kama ambavyo dunia inataka uwe, unaweza kujikuta unajificha nyuma ya mlango kila kukicha, ili uwafurahishe wengine.

Unapowafikiria wasiokuelewa, ndipo unapopoteza mwelekeo. Mawazo haya yanaweza kukupotezea dira katika kila unachofikiria kufanya kwa hofu, iwapo watapenda.

Kinachoifurahisha nafsi yako ndicho sahihi. Hiki kinaweza kuwa msukumo wa wewe kufanikisha mambo mengine katika maisha.

Nafsi iliyoridhika hupata nafasi ya kufungua milango mingine, tofauti na ile inayowaza kuwafurahisha wengine.

Nakumbuka siku moja nilipanda gari la rafiki yangu, kwa bahati mbaya sikuwa napenda aina ya muziki aliokuwa akiupiga. Mara kadhaa nilimwambia toa huo na kila alioubadilisha sikuupenda.

Nilifanya hayo kwa utani, lakini mwisho aliniambia na wewe unakuwa mgumu kufurahisha (entertain). Mwisho aliniambia huo ndiyo aina ya muziki anaoupenda, hivyo kwa kuwa nipo ndani ya gari lake nilipaswa kuusikiliza tu.

Huu ni mfano mdogo, mimi sikutakiwa kuuliza kwa nini anasikiliza aina hiyo ya muziki kwa sababu ndiyo chaguo lake ndani ya himaya yake. Kadhalika akija kwangu itampasa kuusikiliza ule ninaoupenda mimi.

Sawa na mgeni anapokwenda nyumbani kwa mtu, anapaswa kuishi kwa kufuata taratibu za pale na siyo kuanza kujipangia hiki sili, pale silali au hiyo sitaki.

Hapa duniani, kila mtu ana ‘wazimu’ wake, ili maisha yaendelee, kila mtu anapaswa kuuheshimu ‘wendawazimu’ wa mwenzake.

Kuishi kwa kujishtukia ni hatari kwa ustawi wa maisha yako. Hivi unaweza kuwafurahisha watu wangapi dunia hii?

Unapaswa kujua kuwa, tunatakiwa kuishi kwa kuheshimiana kwa maana unapoishia uhuru wako, ndipo unapoanzia wa mwenzako.

Waswahili wanasema; ‘Upungufu ndiyo ubinadamu’. Upungufu wako usikunyime raha kwani kila mtu ana yake.

Lakini, chonde chonde kwa wale wanaojiamini kupita kiasi. Ukiona kujiamini kwako kumepindukia, tambua kuna mahali unaharibu. Jiamini na kuheshimu upungufu wa mwenzako, bila kusahau kukubali kuwa kuna waliokuzidi.

Jiamini kwa kile unachofanya, lakini kujiamini huko kusizidi kipimo. Kama unachofanya hakiwashirikishi wengine, unaweza kufanya unavyojisikia.

Kama ni uamuzi wako binafsi kuhusu mavazi, chakula au starehe yoyote, nadharia hiyo inakubalika bila ubishi, lakini linapokuja suala linalogusa mtu mwingine zaidi au watu, staha ni muhimu.

Vilevile, unapaswa kuheshimu mila na desturi wakati ukifanya mambo yako. Kuheshimu desturi, ndiko huzaa ustaarabu.

Furahia uhuru wako na kila unachokiamini, lakini isiwe kero au kikwazo kwa wenzako. Hata unapokuwa mama au baba wa familia, tabia yako ina mchango katika ustawi wake.

Unaweza kusema uko huru kufanya chochote, lakini je, hakuna anayeathirika na unachokifanya? Kama ni baba uvutaji wa sigara na ulevi uliopindukia hauna athari kwa watoto wako?

Dunia ni yako na maisha ya furaha na Amani ni chaguo Lako!Tumeumbwa na Mungu tumepewa akili na utashi,Ishi maisha yako na usiwe kero kwa wengine!

Na KAKA EMMA
 

 

 

Facebook Comments

You might also like More from author

Leave A Reply

Your email address will not be published.