Mwenyekiti asimamishwa kazi kwa kuchungulia watu usiku

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro amemsimamisha kazi mwenyekiti wa kijiji cha Sayu, kata ya Pandagichiza, Mataifa Balekele (54) baada ya wananchi wa kijiji kudai kuwa mwenyekiti huyo amekuwa na tabia ya kuwachungulia kwenye madirisha nyakati za usiku wakiwa wamelala.


Picha sio ya tukio halisi.

Matiro alikutana na madai hayo katika mkutano wa kijiji hicho jana baada ya kufanya ziara kwa ajili ya kukagua ulimaji wa zao la pamba. Pamoja na kumsimamisha Mkuu huyo wa wilaya alikemea vikali tabia hiyona kusema ni utovu wa maadili.

Aidha katika mkutano Mwenyekiti wa kitongoji Paul Selena aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo. Mkuu huyo wa wilaya alichukua jukumu la kumsimamisha kazi Balekele baada ya baadhi ya wananchi akiwemo Daud Kapela kueleza kuwa mwenyekiti wao huyo amekuwa na tabia ya kuwachungulia kwenye madirisha nyakati za usiku wakiwa wamelala na alipobainika alikubali kosa na kulipa faini.

Akitoa ufafanuzi, mbele ya mkuu wa wilaya, Ofisa Mtendaji wa kata hiyo Denis Kimwaga alisema uamuzi wa kumsimamisha kazi mwenyekiti huyo ulichukuliwa tangu Oktoba mwaka huu baada ya uongozi wa serikali ya kijiji kukaa na kujadili malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai mwenyekiti huyo amekuwa na tabia ya kuchungulia kwenye miji yao nyakati za usiku.

“Kikao hicho kiliridhia mwenyekiti huyo asimamishwe kazi kutokana na tabia hiyo ya kuchungulia kwenye kaya za watu wakiwa wamelala huku yeye mwenyewe akikiri kufanya vitendo hivyo akidai kuwa amepitiwa tu na shetani na kuomba kuwalipa fedha kama fidia watu aliowachungulia,” alieleza Kimwaga.

Hata hivyo, Balekele akizungumza kwa njia ya simu, kwa kuwa hakuwepo mkutanoni alieleza kukubaliana na uamuzi uliofikiwa wa kusimamishwa huku akikataa kujihusisha na tabia ya kuchungulia watu akidai kuwa tuhuma hizo ni chuki binafsi.

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema kuwa mwenyekiti huyo alikuwa amewachosha na tabia zake. “Huyu ni mtu mzima tena kiongozi ambaye ameonesha tabia mbaya, kwani ana familia inayomtegemea kama mke na watoto pamoja na wajukuu imekuwa ni tabia yake ya muda mrefu, amechungulia katika kaya nyingi ambazo wenyewe hawataki kujionesha ni aibu sasa tumechoka kuchunguliwa,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho.

Chanzo: Habarileo

Facebook Comments

You might also like More from author

Leave A Reply

Your email address will not be published.