MATUKIO:Polisi asombwa na mafuriko mpaka kufariki

0

MVUA kubwa inayoendelea kunyesha mfululizo katika maeneo mbalimbali nchini imeendelea kuleta madhara ikiwamo kufariki dunia askari wa Jeshi la Polisi aliyekumbwa na mkasa wa kusombwa na maji yaendayo kasi wakati akiwa na pikipiki visiwani Zanzibar.

 

Aidha, mvua hizo zilizosababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali, yakiwamo ya Tanga na Zanzibar na kusababisha maafa makubwa kwenye baadhi ya maeneo nchini, zimewashtua wabunge ambao jana walitaka kusitishwa kwa shughuli za Bunge ili kupata taarifa kamili na kujadili hatua za kuchukua.

 

KIFO CHA POLISI

Licha ya kuendelea kuharibu miundombinu kama ya barabara na kubomoa nyumba, mafuriko yatokanayo na mvua yaliendelea kuleta vilio baada ya jana kusababisha kifo cha askari wa Jeshi la Polisi, Sajenti Abbas Anas Haji (55). Marehemu alikumbwa na umauti baada ya kusombwa na maji katika barabara ya Fuoni Kibonde Mzungu, Mkoa wa mjini Unguja, Zanzibar.

 

Akizungumza eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 5:30 asubuhi wakati askari huyo akiwa na usafiri wa pikipiki (Vespa), akitokea kazini Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kuelekea nyumbani kwake.

 

Alisema alipofika katika eneo hilo, aliteleza na kuanguka kabla ya kusombwa na maji hayo.

 

Mwandishi wa Nipashe alifika katika eneo la tukio na kukuta umati wa watu waliokuwa wakiendelea na shughuli za uokozi wa mwili wa marehemu ambao ulikuwa hauonekani kutokana na maji mengi yaliyokuwapo.

 

Hata hivyo, vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kuupata mwili wa askari huyo majira ya saa 9:30 jioni.

 

Kamanda Ali alisema marehemu ni wa kitengo cha picha Makao Makuu ya Jeshi hilo, Zanzibar.

 

Alisema eneo hilo ni hatari kutokana na barabara kufunikwa na maji ambapo pembezoni mwa barabara hiyo kuna bonde kubwa la mpunga na maji huwa mengi, yakipita barabarani kwa kasi na mengine kutuwama pembezoni.

 

“Hivi sasa haturuhusu waenda kwa miguu wala vyombo vya moto kupita eneo hilo kwa sababu maji yana kasi kubwa na yanaweza kusababisha maafa mengine,”alisema.

 

Alisema mwili wa marehemu umeshakabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi ambayo yanatarajiwa kufanyika kwao, Fuoni Kibondeni.

 

Alisema Jeshi la Polisi limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha askari huyo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari, hasa katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

 

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B’,Unguja, Silima Ali Haji, alisema hali ya mafuriko ya mvua si nzuri na maeneo mengi yameathirika na mvua hizo, ikiwamo nyumba kujaa maji na pia barabara kutopitika kwa kufunikwa na maji.

 

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni barabara ya Mwanakwerekwe Sokoni ambayo hivi sasa haipitiki, barabara ya Fuoni Kibonde Mzungu na eneo la Tomondo Ziwa Maboga ambako nyumba nyingi hivi sasa zimejaa maji na wananchi waliokuwapo kukosa mahala pa kuishi.

 

“Bado hatujafanya tathmini katika wilaya yangu familia ngapi zimekosa makazi. Lakini athari za mvua ni kubwa na niwasihi wananchi wachukue tahadhari kwani bado mvua zinaendelea kunyesha”alisema.

 

Akizungumzia kuhusu tukio la Mafuriko Bwejuu Mkoa wa Kusini Unguja ambalo limeenea katika mitandao ya kijamii ya kwamba watu wanatembea mitaani kwa mitumbwi, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mafuriko yapo katika baadhi ya maeneo lakini siyo makubwa ya aina hiyo na kwamba, video inayosambazwa haiakisi uhalisia wa eneo husika.

 

Akizungumzia kuhusu maafa ya mvua zinazoendelea kunyesha, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema serikali yake imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuimarisha miundombinu ili kuhimili maafa hayo kwa kuzuia maji yasituwame pasipostahili.

 

“Nimeshuhudia eneo la Tomondo Ziwa Maboga pamejaa maji. Nyumba nyingi zimefukiwa na maji lakini kila wananchi wakitakiwa waondoke hawataki,” alisema Dk. Shein, akisisitiza wananchi kuzingatia tahadhari zinazotolewa kipindi hiki.

 

Aidha, imeelezwa kuwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba zimeathiri nyumba 325 katika Mkoa Kusini Pemba, nyumba 667 kukimbiwa na wakazi wake ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja pamoja na kubomoka kwa miundombinu ya barabara na baadhi ya madaraja.

 

WABUNGE WASHITUSHWA

Katika mjadala wa jana bungeni, wabunge waliitaka serikali kueleza athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini na hatua inazozichukua kuwapa unafuu wa maisha wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo.

 

Mjadala huo ulisababisha Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyekuwa anaongoza kikao cha Bunge, kuitaka serikali itoe tamko kuelezea jambo hilo na hatua zilizochukuliwa.

 

Chenge alilazimika kuamua hivyo baada ya wabunge watatu kusimama kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika, huku baadhi yao wakitaka shughuli za Bunge zisitishwe ili kujadili hoja hiyo waliyotaka ichukuliwe kuwa ni ya dharura.

 

Wabunge walioomba mwongozo wa Kiti cha Spika ni Stephen Ngonyani ‘Prof. Majimarefu’ (Korogwe Vijijini-CCM), James Mbatia (Vunjo-NCCR Mageuzi) na Rashid Shangazi (Mlalo-CCM).

 

Akiwasilisha hoja yake, Prof. Majimarefu alitumia Kanuni ya 68(7) akisema kuna athari kubwa nchini zilizosababishwa na mafuriko nchini.

 

“Kwenye mkoa wangu wa Tanga kumekuwa na maafa. Leo (jana) hii tunavyoongea kuna watu 1,000 hawana chakula, mahali pa kuishi na hawana msaada wowote,” alisema.

 

“Serikali itawasaidiaje hawa watu wakati kamati za afya zikiendelea na utaratibu?” Alihoji.

 

Katika kujenga hoja yake, Shangazi aliyesimama kwa kuzingatia Kanuni ya 47(1), alitaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili wabunge wajadili kuhusu mafuriko hayo.

 

“Sasa hivi katika Mkoa wa Tanga kuna mafuriko makubwa sana. Na jana (juzi) yametokea maporomoko katika Milima ya Usambara, eneo la barabara za Lushoto-Arusha-Mombo, Pangani-Tanga, Mombo kwenda Lushoto na Kilindi-Morogoro zote zilifungwa,” alisema Shangazi.

 

Alisema Mkoa wa Tanga umegeuka kuwa kisiwa ghafla na umepata athari kubwa na kuiomba serikali ilione jambo hilo ni la kimkakati na Wakala wa Barabara (Tanroads) umezidiwa.

 

Mbatia alisema hali ni tete katika mikoa mingi nchini ikiwamo Kilimanjaro, Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Zanzibar kufuatia mafuriko yaliyojitokeza na kuomba utu kuzingatiwa miongoni mwa wabunge kwa kuamua kutenga walau robo saa kujadili suala hilo na kupendekeza hatua za kuchukua.

 

“Tutenge muda wa dakika 15 ama 20 ili tujadili suala hili ambalo ni la maafa. Tunaweza tukatoa majibu sahihi kwa wapigakura wetu,” alisema.

 

Akijibu maombi ya wabunge hao, Chenge, akirejea kanuni, alisema kwa hali anayoiona, haoni kama suala hilo linahitaji kujadiliwa bungeni kwa kipindi hicho.

 

“Ni kweli tukio hili limegusa maeneo mengi, nawapa pole walioguswa kwa namna moja hata nyingine. Naamini Serikali iliyoko humu ndani, itaitolea maelezo wakiangalia nchi nzima,”alisema Chenge.

 

Alisema anaamini serikali italizungumzia vizuri suala hilo kuliko kila mbunge kujisemea katika eneo lake.

 

Akijibu ombi la Prof. Majimarefu, Chenge alisema Kanuni ya 68(7) kuhusu kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika, ina sharti la lazima mwongozo huo uombwe kwa tukio ambalo limetokea mapema bungeni na si nje ya chombo hicho cha kutunga sheria.

 

HALI YA TANGA

Kutoka Tanga, inaelezwa kuwa mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo zinaendelea kuleta athari na hivyo kukata mawasiliano kati ya mikoa ya Kiliamanjaro na Arusha.

 

Zaidi ya magari yameharibika vibaya baada ya kupondwa na mawe makubwa yaliyoporomoka kutoka juu ya milima kwenda barabarani .

 

Mawe hayo yalifunika baadhi ya magari na kufunga kabisa barabara zinazoelekea wilayani Lushoto lakini kwa mujibu wa serikali mpaka jana hali imerudi shwari na magari yameanza kupita.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, alisema jana kuwa magari hayo yameharibika baada ya kuangukiwa na udongo ambao umetoka juu ya milima katika barabara kuu ya kutokaka wilayani Korogwe kuelekea Soni Wilaya ya Lushoto.

 

Alisema katika ajali hiyo watu nane walijeruhiwa vibaya na walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa matibabu na wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kutibiwa.

 

Kamanda Wakulyamba alisema kuwa magari yaliyoharibika kwa kuangukiwa na udongo wa mawe kutoka milimani kuwa ni Toyota Coaster mbili, Toyota

Carina, Noah na Toyota Hilux na kwamba barabara ya kutoka Mombo kwenda Lushoto iliyokuwa imefungwa, sasa imefunguliwa na magari yameanza kupita kwa tahadhari kubwa.

 

Hata hivyo, mawasiliano kati ya Pangani na Tanga mjini yamekatika baada ya daraja kubomoka eneo la Neema jijini Tanga

Facebook Comments

You might also like More from author

Leave A Reply

Your email address will not be published.