DALILI ZA MIMBA KUTUNGA NJE YA MJI WA UZAZI

HILI ni tatizo ambalo linawaathiri wanawake wengi. Kwa kawaida, mimba zinazotungwa nje ya mfuko wa uzazi hazina uwezo wa kukua kuwa mtoto kamili. Mimba hizi ni hatari kwa afya ya mjamzito kwa vile humfanya kupoteza damu nyingi na hatimaye kusababisha kifo asipowahi kutibiwa. Katika mfumo wa uzazi wa mwanamke, kuna sehemu nyingi ambazo kila moja ina umuhimu wake.

 

Ikiwa sehemu mojawapo itapata hitilafu, husababisha athari katika mfumo wa uzazi. Miongoni mwa sehemu muhimu ni ovari ambayo ndiyo sehemu mayai ya uzazi yanapotengenezwa. Mayai haya husafiri kupitia mirija ya fallopian.

 

Kazi za mirija ya fallopian ni kusafirisha mayai kutoka katika kiwanda chake cha uzalishaji (ovari) mpaka kwenye mfuko wa uzazi (uterus). Utungisho wa yai la kike (ovum) na mbegu ya kiume (sperm) hufanyika kwenye mirija hii.

 

Mara baada ya utungisho, misuli inayozunguka mirija ya fallopian ikishirikiana na vinyweleo vilivyopo ndani ya mirija hii husukuma kiinitete au yai lililorutubishwa na kulipeleka kwenye uterus. Yai lililorutubishwa au
kiinitete, lifikapo kwenye uterus hujipachika katika mojawapo ya kuta zake kwa ajili ya kuendelea kurutubishwa, kukua taratibu na hatimaye kufanya mtoto.

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya jicholauswazi

Android ===>Google Play

Inapotokea misuli hii kushindwa kufanya kazi au vinyweleo hivi kukosekana, kiinitete hushindwa kusafirishwa kuingia kwenye uterus na hivyo hujitunga nje ya uterus na kusababisha hali ya ectopic pregnancy. Karibu asilimia 1-2% ya mayai yaliyorutubishwa hutunga nje ya mfuko wa uzazi wa mwanamke. Aidha, zaidi ya asilimia 95% ya mimba zinazotunga nje ya Uterus hutokea kwenye mrija wa Fallopian.

 

Mimba zinazotunga kwenye mrija huo husababisha kiinitete (embryo) kujipachika katika kuta zake na hivyo kusababisha mishipa ya damu inayopita karibu na mrija wa fallopian kupasuka na damu kutoka kwa wingi, hali ambayo isiposhughulikiwa mapema husababisha madhara zaidi na hata kifo.

 

Kuna aina kuu nne za mimba zinazotunga nje ya mfuko wa uzazi; mimba zinazotunga kwenye mirija ya fallopian, zinazotunga nje ya uterus na nje ya mirija ya fallopian, zinazotunga ndani na nje ya uterus kwa wakati mmoja na
zinazojirudia kutunga nje ya mfuko wa uzazi. Inapotokea yai moja limepandikizwa nje ya uterus na jingine ndani ya uterus, uwezekano mkubwa ni kwamba yai lililotungwa ndani ya uterus litakuwa na kutoa mtoto.

 

Wakati fulani hutokea kuwa, hata baada ya oparesheni ya kuondoa mimba iliyotunga nje ya kizazi kufanyika, baada ya muda fulani seli za kiinitete huendelea kukua na kujitengeneza tena kufanya kusanyiko la seli kama mimba nyingine. Hali hii huitwa mimba zinazoendelea kutunga nje ya mfuko wa uzazi, kitaalamu persistent ectopic pregnancy. Sababu nyingine za mimba kutunga nje ya mji wa mimba ni mjamzito kuwa na matatizo katika mirija ya fallopian.

 

Magonjwa yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke (PID), matumizi ya vitanzi vya kuzuia mimba (Intra-uterine contraceptive devices), kuoteana kwa tishu za uterus kwenye viungo vingine vya uzazi au endometriosis. Uvutaji sigara Uvutaji sigara kwa mwanamke una uhusiano mkubwa na utungaji wa mimba nje ya kizazi. Imeonekana kwamba wanawake
wanaopendelea kuvuta sigara mara kwa mara wana hatari ya kupatwa na tatizo hili mara tano zaidi ya wale wasiovuta kabisa.

 

Hali hii husababishwa na ‘nicotine’ iliyomo ndani ya tumbaku. Kwa kawaida nicotine huchochea kusinyaa kwa mirija ya fallopian hali iletayo kuziba kwa mirija hiyo na hivyo kufanya kiinitete kushindwa kupita kwenye mirija kuingia kwenye uterus na kufanya mimba kutunga kwenye mirija ya fallopian.

 

Oparesheni yoyote inayohusu mirija ya fallopian inaongeza uwezekano wa mwanamke kutunga mimba nje ya uterus kwa vile mirija ya fallopian huwa imesinyaa kutokana na oparesheni hiyo. Matumizi holela ya baadhi ya dawa Matumizi ya baadhi ya dawa zenye homoni husababisha kupungua kwa uwezo wa mirija ya fallopian kusukuma kiinitete kuelekea kwenye uterus na hivyo kuleta uwezekano wa utungaji wa mimba nje ya kizazi. Dawa hizo ni kama dawa za kuzuia mimba zenye homoni za kike za progesterone, na dawa za kusaidia uzazi aina ya clomiphene.

 

DALILI ZAKE

 

Katika wiki za mwanzo za ujauzito, mimba iliyotunga nje ya uterus huwa na dalili sawa na za mimba ya kawaida. Dalili hizi ni pamoja na mwanamke kukosa hedhi, kujaa kwa matiti, kichefuchefu, na uchovu wa mwili. Hali hii hufanya ugunduzi wa mimba iliyotunga nje ya uterus kuwa mgumu katika hatua zake za awali. Hata hivyo, dalili ya awali ya kuonesha kuwa mimba imetunga nje ya kizazi ni kuwepo kwa maumivu makali na damu kutoka ukeni. Maumivu yanaweza kuwa kwenye nyonga, tumbo au wakati mwingine kwenye mabega au shingo (iwapo kiwango cha damu inayotoka kwenye mirija iliyopasuka ni kingi sana mpaka kugusa kiwambo cha hewa).

 

Maumivu haya huweza kuwa makali na yanayokata kama kisu na yanaweza kuwa upande mmoja zaidi wa nyonga ingawa si lazima yawe upande ulio na mimba. Dalili nyingine ni mjamzito kuwa na kizunguzungu na kuzimia kwa sababu ya kupoteza damu kwa wingi, shinikizo la damu kuwa chini na maumivu ya chini ya mgongo. Unapoona dalili hizi, unashauriwa kuwahi hospitali haraka.

Facebook Comments

You might also like More from author

Leave A Reply

Your email address will not be published.